Posted On: October 26th 2026, 09:26 pm
Mkuu wa Mkoa wa Iringa,
@comradekheri amewataka viongozi wa vijiji vinavyozunguka mradi wa umeme wa upepo katika Kijiji cha Usokami, Wilaya ya Mufindi, kuhamasisha wananchi kushiriki katika kulinda miundombinu ya mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 3.9, huku akiwahimiza kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme kuimarisha shughuli za kiuchumi na kujikwamua kimaisha.
Akizungumza leo Oktoba 26,2026 wakati wa kutembelea mradi huo katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano ya kutembelea viwanda mkoani Iringa, Mhe. Kheri amesema kuwa uwekezaji huo una manufaa makubwa kwa jamii, ikizingatiwa kuwa unawanufaisha wananchi zaidi ya 9,000 kutoka vijiji 32 katika kata sita za Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi akisema kuwa ni muhimu wananchi kuutunza mradi huo ili uendelee kutoa huduma ya umeme na kuchochea shughuli za uzalishaji, biashara na maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya Mwenge Hydro Power Ltd, Deogratius Massawe, amesema kuwa kampuni hiyo inayotekeleza mradi huo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme ya uhakika na kwa gharama nafuu, ili kuongeza fursa za kiuchumi, kuimarisha shughuli za uzalishaji na biashara, pamoja na kuchochea maendeleo ya jamii zinazozunguka mradi huo.
Naye Michael Mahenge, akizungumza kwa niaba ya wananchi wanufaika, amesema mradi huo umeleta mabadiliko chanya katika maisha yao kwa kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo hapo awali zilikuwa ngumu kutekelezwa kutokana na changamoto ya upatikanaji wa umeme.
Amesema kuwa uwepo wa umeme huo umewawezesha wananchi kuanza kufanya shughuli ndogo ndogo za uzalishaji ndani ya kijiji hicho, ikiwemo kusaga mahindi, hali inayorahisisha upatikanaji wa huduma, kupunguza usumbufu na kufungua fursa za kuongeza kipato kwa wananchi.