Instagram story viewer> @voicemediatz> Post
6 days ago
Co Creator: mdetele_jr
1
Posted On: October 30th 2026, 11:43 am
Tagged Users:
Wahitimu wa Shule ya Sekondari Uwemba iliyopo Wilaya ya Njombe, mkoani Njombe, wamechangia mahitaji mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili kwa ajili ya kusaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 775.

Mchango huo ni sehemu ya jitihada za wahitimu hao kurejesha kwa jamii kupitia taasisi iliyowapatia msingi wa elimu, huku ukilenga kuunga mkono juhudi za kuboresha mazingira ya shule na kuimarisha upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Oktoba 29, 2026 shuleni hapo Mratibu Mkuu wa Alumni, Casmill Mdetele, amesema uamuzi wa kurejea shuleni hapo umetokana na dhamira ya kuthamini mchango wa taasisi hiyo katika maisha yao na kushiriki katika maendeleo yake.

Mdetele amewahimiza wahitimu wengine kujenga utamaduni wa kutembelea shule walizosoma na kuchangia maendeleo yake, akieleza kuwa ushiriki wa wahitimu ni muhimu katika kusaidia kukabiliana na changamoto zinazozikabili taasisi za elimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Jonisia Ngailo, ameishukuru Alumni kwa mchango huo, akibainisha kuwa utasaidia shule katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Hata hivyo, amesema bado shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji nguvu za pamoja, huku akitoa wito kwa wahitimu wengine, taasisi na wadau wa elimu kuendelea kujitokeza kuunga mkono maendeleo ya shule hiyo.

Hatua hiyo inadhihirisha umuhimu wa ushirikiano kati ya shule na wahitimu wake katika kuimarisha mazingira ya elimu na kutoa fursa bora zaidi kwa kizazi kinachoendelea kupata maarifa.
Comments (1)
kimwanyascents.tz 6 days ago

More posts

back to up