Posted On: November 2nd 2026, 05:23 pm
Leo Mahakama kuu ya Kenya imesikiliza kesi ya kutekwa kwa Mwanaharakati wa Tanzania, Twaha Mwaipaya jijini Nairobi mnamo tarehe 25 October 2026. Katika kesi hiyo Inspekta Jenerali wa Polisi nchini humo, Douglas Kanja, na Mwanasheria mkuu wa serikali waliburuzwa mahakamani hapo kueleza alipo Twaha.
Polisi wamejitetea kwamba hawamshikilii Twaha na wala hawajui alipo. Hata hivyo pamoja na utetezi huo, Jaji wa Mahakama Kuu Alexander Muteti amemtaka IGP Kanja kueleza ni wapi alipo Twaha Mwaipaya ikiwa Polisi hawapo nae. Jaji Muteti amesema ni jukumu la Polisi kulinda raia na mali zao, hivyo kama hawamshikilii Twaha basi waseme anashikiliwa na nani. Kushindwa kufanya hivyo ni kushindwa kutekeleza wajibu wao kisheria.
Katika kesi ya maombi ya Habeas Corpus inayotaka Mwaipaya afikishwe Mahakamani au mamlaka zieleze alipo, Jaji Muteti amelitaka jeshi la Polisi kuwasiliana na kampuni za simu ili kupata taarifa zinazoweza kusaidia kumpata Twaha. Hata hivyo Wakili wa Serikali Christopher Marwa, amesema tayari Polisi wameomba taarifa za Twaha kutoka kwenye mtandao aliokua anatumia, lakini bado mtandao huo haujawapa polisi taarifa hizo.!
Load More