Posted On: October 14th 2026, 08:36 pm
Wananchi mkoani Tabora wamehimizwa kujiunga na huduma ya umeme na kutumia nishati safi ya kupikia, ikiwemo majiko ya umeme, kwa lengo la kuboresha afya, kutunza mazingira na kuinua maisha yao ya kila siku. Rai hiyo imetolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia ziara ya kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuhusu miradi ya nishati vijijini.
Kupitia ziara hiyo, wananchi wanapatiwa elimu kuhusu taratibu za kuomba kuunganishiwa umeme, matumizi sahihi na yenye tija ya nishati, pamoja na tahadhari za kiusalama wanazopaswa kuzingatia wanapotumia umeme majumbani na katika shughuli za kiuchumi. Aidha, wanahimizwa kutumia nishati safi ya kupikia ili kupunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi na uchafuzi wa mazingira.
Vilevile, wananchi wametakiwa kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa kwa kukumbatia nishati safi ya kupikia, pamoja na kushiriki katika kutunza miundombinu ya umeme. Juhudi hizo za REA zinalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma za nishati vijijini na kuhakikisha nishati inatumika kwa usalama, ufanisi na kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira.
#DigitalnewstzUPDATES