Posted On: October 30th 2026, 08:02 pm
RAIS SAMIA AZINDUA OFISI NA BARABARA ZA LAMI MTUMBA, ASISITIZA UFANISI NA UWAJIBIKAJI SERIKALINI.
DODOMA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka watumishi wa umma kuhakikisha uwekezaji wa Serikali katika ofisi na miundombinu ya kazi unaongeza ufanisi na kuboresha huduma kwa wananchi.
Rais Samia ameyasema hayo leo Oktoba 30, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Majengo ya Ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali, pamoja na Barabara za Lami katika Mji wa Serikali Mtumba, mkoani Dodoma, akiwa ameambatana na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço, aliyehitimisha ziara yake ya kitaifa nchini leo.
Miongoni mwa viongozi walioshiriki uzinduzi huo ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (Mb.), na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Athuman Katimba (Mb.), pamoja na viongozi wengine wa Serikali.
Rais Samia aliwataka watumishi wa umma kuzingatia sheria na taratibu katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa mazingira bora ya kazi yanapaswa kuendana na uwajibikaji na huduma bora.
Rais Samia amewashukuru waasisi, Marais waliomtangulia, watumishi wa Serikali na sekta binafsi kwa mchango wao katika ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba. Kipekee, alitambua mchango wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ya kuhamishia shughuli za Serikali mkoani Dodoma.
Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço amesema urafiki kati ya Angola na Tanzania unapaswa kuzaa fursa za biashara, ajira na uwekezaji kwa wananchi.